Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema mara baada ya taarifa ya awali ya dalili za uwezekano wa uwepo wa El Nino ulipotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini – TMA, Ofisi ya Waziri Mkuu imetekeleza na kuratibu hatua kadhaa za kimsingi na za awali.

Mhagama ameyasema hayo hii leo Oktoba 13, 2023 jijini Dodoma wakati Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko akizindua Mpango wa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini.

Amesema, hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha wanawasilisha taarifa kwenye wizara na mikoa hasa mikoa husika ili kufanya tathmini ya maeneo yanayoweza kuathirika na kuandaa mipango ya hatua za kuzuia au kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, aliishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini.

Alisema, matukio ya hali mbaya ya hewa ambayo yanaendelea kuongezeka ni pamoja na mvua kubwa za muda mfupi, joto kali, upepo mkali na vimbunga ambapo tathmini ya karibuni inaonesha matukio ya El Nino yataongezeka kwa idadi na ukubwa kadri ambavyo joto la dunia linaendelea kuongezeka.

Chelsea kumng'oa Victor Osimhen SSC Napoli
Kocha Tanzanite Queens aanika mipango ya kufuzu