Uongozi wa Klabu ya Geita Gold FC umeripotiwa kuwa katika mazungumzo ya kumuongezea mkataba mshambuliaji wa timu hiyo, Elias Maguri baada ya msimu kwisha.
Nyota huyo aliyewika na timu mbalimbali zikiwamo Simba SC, Platinum, KMC na AS Kigali alisaini mkataba wa miezi sita katika Dirisha Dogo la Januari, mwaka huu baada ya kukaa nje ya uwanja tangu alipoachana na Ruvu Shooting msimu uliopita.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo zililidokeza kuwa kuwa sababu kubwa ni kutokana na kiwango kizuri ambacho nyota huyo ameonyesha.
“Mkataba wa awali mwanzo ulikuwa ni kama wa majaribio kwa sababu alikaa nje kwa muda mrefu, hivyo tusingeweza kumuamini moja kwa moja. Uwezo wake umetufanya kukaa naye chini ili kuzungumzia maslahi mapya kwa manufaa yetu,” kimeeleza chanzo hicho
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Leonard Bugomola amesema kwa sasa malengo yao ni kumalizia michezo iliyobaki na kama mazungumzo ya mkataba mpya yatakuwepo baina yao na mchezaji watayaweka wazi pindi muda utakapofika.
Kwa upande wake Maguri amesema hajui jambo lolote linaloendelea juu ya kuongezewa mkataba, lakini kikubwa anachofanya ni kuendelea kufanya vizuri na pindi msimu utakapomalizika ndipo atakuwa na majibu sahihi ya kutoa kuhusu hatima yake.
Bao moja alilolifunga katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Uhuru, limemfanya kufikisha matano akiwa ndiye kinara ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Fredy Felix Minziro.