Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Umma na Binafsi katika kushiriki Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa Agosti Mosi, 2023 na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango yanatarajia kufikia kilele chake tarehe 8, 2023 ambapo Mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika maadhimisho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya ofisi hiyo ikiwemo elimu masuala ya Muungano na Hifadhi ya Mazingira kupitia Maafisa wa Idara hizo ambao wanatoa ufafanuzi na kujibu maswali mbalimbali ya wateja wanaotembelea banda hilo.
Aidha, katika kuhakikisha elimu ya masuala ya Muungano na Mazingira inawafikia walengwa, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia maonesho hayo imeandaa machapisho mbalimbali ikiwemo vipeperushi, magazeti ya zamani yanayohusu historia ya waasisi wa taifa na masuala mengine ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.