Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema madhumuni ya kongamano la kujengewa uelewa juu ya madhara yatokanayo na sauti zilizozidi viwango katika nyumba za ibada ni kuwakutanisha pamoja viongozi wa dini na mila, ili kutoa elimu ya athari ya tatizo hilo kwenye nyumba za ibada na jamii.
Amesema kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015 zimeainisha viwango vinavyoruhusiwa katika maeneo ya makazi, nyumba za ibada, biashara, viwanda na hospitali kwa ajili ya jamii, mfano viwango vya sauti vinavyoruhusiwa katika nyumba za ibada zilizopo maeneo ya makazi ni dBA 60 wakati wa mchana na usiku dBA 40.
“Sauti zinazozidi viwango katika nyumba za ibada zinaweza kuathiri afya za waumini waliopo kwenye nyumba za ibada na maeneo ya jirani na kusababisha matatizo ya kusikia, usingizi na kuathiri uwezo wa kufanya kazi pamoja na kusababisha migogoro kati ya wakazi na viongozi au waumini,” amesema Gwamaka.
Awali, Katibu Mkuu wa JMAT, Askofu Dkt. Israel Maasa alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wenzake wa dini mbalimbali nchini kwa kuendelea kushirikiana hali inayolifanya Taifa liendelee kuwa kitovu cha amani na utulivu.