Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza mchakato wa ujenzi wa vituo vya Mafunzo ya Amali vitakavyojengwa Unguja na Pemba, ili kuwasaidia Wanafunzi watakaokosa sifa za kujiunga na Elimu ya juu kujiendeleza na kupata ujuzi mbali mbali.
Akihutubia katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 59 ya Elimu bila ya malipo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali imekusudia kujenga vituo vitano vya Mafunzo ya Amali sambamba na kujenga Chuo cha ubaharia katika eneo la Bait el Ras Zanzibar.
Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na hatua mbali mbali za upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika katika kujifunza na kufundishia, kuzindua mradi mkubwa wa kuimarisha ubora wa elimu ya lazima na kuwajengea Walimu mbinu na uwezo wa kusomeshea, ili kupata matokeo bora.
Hemed ameeleza kuwa miongoni mwa matunda ya mapinduzi ya mwaka 1964 ni kuondoa ubaguzi na kuleta usawa katika upatikanaji wa elimu kwa wote bila ya kujali itikadi, rangi, kabila, dini na uwezo wa kiuchumi.
Mwaka wa fedha 2023- 2024 Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imejipanga kujenga Skuli ishirini na sita (26) za ghorofa kwa Unguja na Pemba, ambazo zitatatua changamoto ya uhaba wa madarasa, msongamano wa wanafunzi visiwa vidogo vya Tumbatu na Kojani Pemba.
Hata hivyo, amewapongeza Wananchi wa Zanzibar kwa kuthamini juhudi zinazochukuliwa na serikali kwa kuanzisha ujenzi wa skuli na madarasa kwa kujitolea pamoja na kuanzisha miradi ambayo Serikali imechukua hatua ya kukamilisha ujenzi hio.