Wadau wa maendeleo nchini, wameombwa kushiriki katika uchangiaji wa maendeleo ya elimu kwa kutoa kiasi cha fedha kitakachoiwezesha Serikali kukidhi kigezo cha kupata ufadhili wa zaidi ya dola za Marekani milioni 50, kupitia Multplier Grant 2023.
Ombi hilo, limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa za Mitaa, Angellah Kairuki kwa wadau wa elimu Mkoa wa Dar es Salaam kwenye kikao kazi kilicholenga kuwajengea uelewa kuhusu dhana ya GEP LANES MULTIPLIER GRANT na kuwashawishi kuchangia maendeleo ya elimumsingi.
Amesema, endapo Tanzania itaweza kupata ufadhili huo fedha zake zitachangia katika kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango mipya endelevu iliyoibuliwa na mabadiliko ya Sera na Mitaala ya Elimu hususani katika kufanikisha utekelezaji wa eneo la Mafunzo ya Amali.
“Kupitia ufadhili wa GPE Multiplier nchi 18 zimetengewa dola za Marekani milioni 50 kiwango cha juu cha mgao ‘Maximum Allocation’ kwa Mwaka 2023 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo lakini fedha hizo zitatolewa kama nchi itakidhi kigezo cha wadau elimu nchini kuchangia,” amesema Kairuki.