Serikali Nchini imefanya maboresho kwenye baadhi ya maeneo katika Sera ya Elimu na Mafunzo ili kutoa elimu ya ujuzi badala ya elimu ya taaluma pekee ambapo elimu ya lazima itakuwa ya miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa.
Akitoa taarifa kuhusu maboresho hayo hii leo Novemba 2, 2023 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa maboresho hayo utaanza mwaka 2027 sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba na badala yake kuanza kufanyika kwa tathmini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari.
Amesema, hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika kwa changamoto mbalimbali zikiwemo, mfumo wa elimu kujikita zaidi kwenye elimu ya jumla na kukosa fursa za elimu na mafunzo kwa kuzingatia mahitaji na njia mbalimbali za ujifunzaji kutokidhi kulingana na mazingira.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni “Mitaala kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, mfumo usio fanisi wa udhibiti na ithibati ya elimu na upungufu wa nguvu kazi. Changamoto hizo zilizaa hitaji la kuboresha sera yetu ya elimu ili kukidhi mahitaji ya sasa na wakati ujao.”
Akifafanua kuhusu maeneo yaliyoboreshwa kwenye sera hiyo ambayo tarehe ya uzinduzi wake itatangazwa baadaye Majaliwa amesema, “Sera ya Elimu na Mafunzo imefanyiwa mabadiliko kwenye maeneo kadhaa ikilinganishwa na sera iliyopita kwa kuongeza fursa za elimu ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) ambayo itaanza kutolewa kuanzia kidato cha kwanza.”
Waziri Mkuu, alikuwa akitoa taarifa kuhusu kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma.