Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema mpaka sasa imetumia zaidi ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya bunifu 200 ambazo zimebuniwa na wabunifu mbalimbali kupitia mashindano ya Kitaifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu ( MAKISATU).
Hayo yameelezwa leo Mei 4 2022 Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof.Eliamani Sedoyeka wakati akiwajengea uwezo wa Waandishi wa Habari kuhusu masuala ya kibunifu na Kuelekea wiki ya Ubunifu nchini itakayoanza Mei 15-20 mwaka huu.
Prof. Sedoyeka amesema kwa mwaka huu zaidi ya shilingi bilioni moja zitatumika kutafuta na kuvumbua vipaji mbalimbali katika Mikoa 16.
Aidha ameongeza kuwa mwaka ujao watatumia zaidi ya shilingi bilioni 5.5 kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuibua na kuendeleza bunifu mbalimbali.
Katibu Mkuu huyo amesema Sayansi na teknolojia ni muhimu sana katika dunia ya sasa kwa sababu inachochea maendeleo kwa kasi kubwa hivyo kwa kuwapatia Wanahabari mafunzo kuhusu Ubunifu itakuwa njia rahisi kwa jamii kupata taarifa kupitia vyombo vya habari.
“Ubunifu na Ujuzi ni moja kati ya mambo yanayowachanganya watu sana imekuwa ngumu sana kwao kuyatofautisha ama kuyafananisha haya maneno mawili hivyo kupitia haya mafunzo na majadiliano mtakayoyafanya leo kuelekea wiki ya Ubunifu Tanzania mwaka 2022 naamini jamii itapata elimu ya kutosha kwa sababu mtakuwa mnazungumza mambo mnayoyajua kiundani,” amesema Prof.Sedoyeka
Prof.Sedoyeka ameongeza kuwa dunia hivi sasa ipo katika mapinduzi ya nne ya viwanda hivyo kupitia mapinduzi hayo nguvu ya Sayansi na Teknolojia imekuwa kubwa hasa katika eneo la ubunifu ambapo hiyo inadhihirisha kukuwa kwa Teknolojia.
“Kama taifa ni lazima tuende na kasi hii ya dunia hivyo kupitia mapinduzi haya ya nne ya viwanda ni lazima kutengeneza wabunifu wengi na hii inajidhirisha kwa sababu hata kwa sasa Tanzania imekuwa kimbilio la nchi za jirani kwa sababu ya Bunifu zetu mfano Bunifu katika taasisi ya Moyo ya Jakaya na Taasisi ya Mifupa (MOI) imekuwa kimbilio ,wagonjwa wengi wanatoka nje ya nchi kuja kupata Matibabu nchini na hiyo ndio nguvu za Ubunifu,” amesema Prof.Sedoyeka.
Kwa upande wake Prof.Maulilio Kipanyula ambaye ni Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu amaesema kuwa kauli mbiu ya Wiki ya MAKISATU itakuwa ni “Ubunifu kwa maendeleo endelevu” itakwenda pamoja na majadiliano mbalimbali kwa njia ya Semina na mafunzo kwa Wabunifu ya Kijasiriamali na kuwapa nafasi wabunifu kuonesha bunifu zao .
Akiongea kwa niaba ya waandishi wa habari Sakina Abdulmasoud ambae pia ni balozi wa mazingira amesema semina hiyo itawasaidia waandishi wa habari katika habari zao kutaarifu umma juu ya masuala ya kibunifu huku akitumia nafasi hiyo kuwakumbusha kuwa masuala ya Kibunifu yanakwenda sambamba na utunzaji wa Mazingira.