Kampuni ya Ellipsis Digital imezindua rasmi programu ya kufundisha bure utengenezaji wa programu za kompyuta nchini Tanzania, ambapo programu hiyo imeundwa ili kujenga mahusiano na watengenezaji wa programu za kompyuta ambazo ni maalumu kwa vijana ambao watahitaji kujiunga ili kupatiwa mafunzo kwa vitendo.
Kampuni hiyo imepanga kutoa ujuzi huo wa kutengeneza programu za kompyuta kwa njia ya masomo yaliyopangwa kwa umakini wa hali ya juu ili kuendana na ongezeko la uhitaji wa watengenezaji wa programu za kompyuta duniani.
Ellipsis Digital imepokea maombi mengi ya wahitaji wa kujifunza utengezaji wa programu za kompyuta lakini wataanza na wanafunzi 20 tu, huku mkazo ukiwekwa kwa wanafunzi 6 tu kwa mwaka 2019 watakaofanya vizuri kwenye mafunzo ya awali.
”Tunafundisha watengenezaji wawili wa programu, kila wakati wateja wetu wakiajiri mmoja wao, na hii ni muhimu kwa sababu Tanzania ina asilimia zaidi ya 44 ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 na hii ina maana vijana milioni 20 nchini Tanzania watahitaji ajira mpya katika miaka mitatu hadi mitano ijayo, kwa hiyo Ellipsis Digital inatoa nafasi hii ya kipekee kwa Watanzania ili waweze kushindana katika masoko ya kimataifa pia,”amesema mmoja wa wafanyakazi wa Ellipsis Digital
Aidha, kampuni hiyo imezindua tovuti yao ambayo inajumuisha habari zote muhimu kuhusu jinsi ya kushirikiana nao au kuajiri watengenezaji wa programu kwa ajili ya kampuni au biashara ya mtu husika.
Tovuti hii inapatikana kwa kutembelea www.ellipsis.co.tz
Kampuni ya Ellipsis Digital ilianzishwa mwaka 2018 huko Wels, Austria na wajasiriamali wa teknolojia, mmoja mwenye asili ya Tanzania na mwingine mwenye asili ya Austria, ambapo wawili hao walisajili rasmi kampuni hiyo mnamo tarehe 2 Januari 2019 jijini Dar es Salaam, Tanzania na ofisi kuu za Ellipsis Digital ziko mtaa wa Samora huku wakiwa na wawakilishi nchini Austria, Sweden na Uholanzi.
Ellipsis Digital huajiri vipaji katika sekta ya utengenezaji wa programu za kompyuta na hufanya kazi kwenye miradi kutoka Ulaya na maeneo mengine duniani na huwa wanawaendeleza watengenezaji wao wanaowaajiri kwa kupitia mafunzo na warsha mbalimbali.