Kiungo kutoka nchini Argentina na klabu ya Norwich City Emiliano Buendía Stati, anaamini klabu ya Arsenal haitafanikisha lengo la kumsajili katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, na badala yake ataendelea kusalia Carrow Road, hadi mwishoni mwa msimu huu.
Arsenal wanatajwa kujipanga kumsajili kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24, ambaye kiwango chake kimekua gumzo nchini England na inasemekana huenda kikasaidia kuirejesha Ligi Kuu ya England Norwich City.
Buendía amekuwa akitajwa kama mbadala wa Mesut Ozil, ambaye kwa sasa yuko Uturuki akikamilisha uhamisho wake kwenda Fenerbahce, akitokea Emirates Stadium yalipo makao makuu ya The Gunners.
Wakati kiungo huyo akipewa nafasi kubwa ya kucheza Ligi Kuu ya England kwa kusajiliwa na Arsenal, vyanzo vya karibu na mchezaji huyo vinaeleza kuwa, kwa sasa amejikita zaidi katika kuisaidia Norwich City ili itimize lengo la kurejea kwenye Ligi pendwa ya ‘PL’.
Wawakilishi wa mchezaji huyo, ambao pia Walikuwa wawakilishi wa Emiliano Martinez, wana uhusiano mzuri na Arsenal na wana mkataba wa kawaida wa kufanya Biashara na mkurugenzi wa ufundi wa The Gunners, Edu.
Kwa msimu huu wa 2020/21 Buendía amshafumania nyavu mara saba, huku akitoa pasi za mabao sita, huku Norwich City ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza nchini England ‘Championship’ kwa alama nne zaidi ya wapinzani wao wa karibu Swansea City.