Mlinda Lango wa Mabingwa wa Dunia ‘Timu ya Taifa ya Argentina’ na Klabu ya Aston Villa ya England, Emiliano Martinez huenda akatimkia kwa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, wanaonolewa na Meneja Julian Nagelsmann.
Martinez mwenye umri wa miaka 30, ambaye alikuwa kwa muda wa mkopo na timu kama Oxford, Sheffield Wednesday na Rotherham wakati wa akiwa Mwajiriwa wa Klabu ya Arsenal, alitajwa kuwa Mlinda Lango Bora wa Fainali za Kombe la Dunia zilizofikia tamati Jumapili (Desemba 18), nchini Qatar.
Kando na hayo, Mlinda Lango huyo katika dakika za lala salama dhidi ya Australia na Ufaransa, Martinez alikuwa shujaa wa mikwaju miwili ya penalti dhidi ya Uholanzi na Ufaransa.
FC Bayern Munich wanatamani sana kuimarisha safu yao ya Walinda Lango wakati wa Dirisha Dogo la Usajili, kufuatia Manuel Neuer kuvunjika mguu baada kurejea nyumbani akitokea Qatar kwenye Kombe la Dunia.
Ingawa itakuwa ngumu kwa Muargentina huyo kukataa soka ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Villa hawana shinikizo la kumuuza na amepewa mkataba hadi msimu wa majira ya joto wa 2027.
Bado wakala wa mchezaji huyo, Gustavo Goni, amebatilisha uvumi huo na baadhi ya maoni ya kutiliwa shaka kwa vyombo vya habari vya Italia mwishoni mwa juma.
Alipoulizwa kama mteja wake atafikiria kuhamia Serie A, Goni alijibu: “Leo kuna timu chache ambazo zinaweza kumudu kipa kama yeye.”