Mlinda Lango wa Argentina, Emiliano Martinez anamuona Mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe kama mshindi wa miaka ijayo wa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia ‘Ballon dOr’ huku akieleza namna alivyoshindana na fowadi huyo wa kimataifa wa Ufaransa wakati wa Kombe la Dunia.
Mlinda Lango huyo wa Argentina alijikuta kwenye utata baada ya kuonekana akiwa ameshikilia mwanasesere mwenye uso wa Mbappe wakati wa gwaride la kusherehekea ushindi wa Kombe la Dunia 2022.
Aidha, inadaiwa pia aliwakusanya wachezaji wenzake kwenye chumba cha kubadilishia nguo baada ya kuifunga Ufaransa katika fainali ya Kombe la Dunia 2022 na kuimba wimbo ambao ulikuwa ukilenga kumpiga vijembe fowadi huyo ambaye alipachika mabao matatu dhidi yake kwenye fainali hiyo.
“Sio bure kwamba anachukuliwa kuwa mmoja kati ya wachezaji bora zaidi ulimwenguni. Ninamheshimu kama mchezaji na kama mwanaume,” aliliambia Jarida la L’Equipe baada ya kukusanya Yachine Trophy kwa kuchaguliwa kuwa kipa bora wa mwaka.
“Kylian ni mfano wa kuigwa. Ni mtu poa sana. Kushinda Kombe la Dunia, kucheza fainali ijayo na kufunga hat-trick… Wafaransa wote wanapaswa kujivunia kuwa na mchezaji kama yeye. Wakati Leo (Messi) na (Cristiano) Ronaldo watastaafu, Kylian atafuata njia zao.”
Ingawa Mbappe alionekana kuchanganyikiwa baada ya kukosa tuzo, alionyesha kiwango chake kwa kutuma ujumbe wa ‘unastahili’ kwa Messi baada ya Muajentina huyo kunyakua tuzo ya nane ya ‘Ballon d’Or ambayo ilimfanya kuweka rekodi huko Paris mwanzoni mwa juma hili.