Mmoja wa mabosi wa Real Madrid, Emilio Butragueno amesema hawatawadharau wapinzani wao baada ya kupangiwa SSC Napoli katika Kundi C la Ligi Mabingwa Ulaya.

Real Madrid itamenyana pia na Union Berlin na Braga, lakini bosi huyo anaihofia SSC Napoli kwa sababu ilikuwa hatari msimu uliopita.

Butragueno alisema: “Ni kundi gumu. Tunajua mashindano haya yalivyo. Kila mechi ni changamoto na itabidi tucheze kwa kiwango cha juu ili tufike hatua inayofuata. SSC Napoli ilikuwa na msimu mzuri mwaka jana.

“SSC Napoli ina wachezaji hatari na watakuwa wapinzani wagumu. Braga na Union Berlin ni timu ambazo hatujawahi kucheza nazo. Pia ni timu mbili zenye ushindani mkubwa na haitakuvwa rahisi.”

Real Madrid ina historia nzuri ya Ligi Mabingwa Ulaya kwani ndio inaongoza kwa kunyakua taji hilo mara 14.

Msimu uliopita ilishindwa kutoboa mbele ya Manchester City katika mechi ya Nusu Fainali, lakini msimu huu itajipanga kuhakikisha inafika mbali katika michuano hiyo na hatimaye kubeba taji kwa mara ya 15.

“Real Madrid ina ushindani mkali katika michuano hii. Licha ya kuwa na wachezaji majeruhi waliopo kikosini tunaamini watashinda vikwazo hivyo. Tunajivunia wachezaji wetu. Unapovaa jezi ya Madrid inamaanisha mambo mengi sana katika historia ya klabu hii,” alisema.

Hersi Said: Tutaweka rekodi mpya Afrika
Azam FC kuitumia AFCON 2024