Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM Eng. Hersi Said amewashukia baadhi ya wadau wa soka nchini Tanzania walioibua hoja inayogusa udhamini wa kampuni hiyo kwenye klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hoja hiyo imeibuka kufuatia Kampuni ya GSM kuwa mdhamini ya Young Africans, Namungo FC na Coastal Union, huku ikijaribu kuisafirisha Biashara Utd kwenda Libya (safari ambayo ilishindikana).
Wasiwasi uliopo ni kwamba kama kampuni ya GSM imewekeza kwenye klabu zaidi ya moja itakua na sababu ya kushawishi upangaji wa matokeo hasa kwa timu wanazozidhamini zitakapokutana.
Hersi ameandika kuwa: ”Timu hizi zinajiendesha kwa hasara kwa miaka mingi ndio maana zimekwama. Ukisema hivi mtu anaweza asikuelewe lakini ukitazama mapato ya klabu na matumizi ndio utajua kwanini zinajiendesha kwa hasara”
”Yanga inalipa mishahara yenyewe, ina mifumo yake ya kuajiri watu sisi tuna-support tu. Yanga ni timu kubwa huwezi kufananisha na hawa makolo. Huwezi kumleta mchezaji kama Bangala halafu hajui mshahara analipwa na nani”
”Hii ni klabu kubwa, tunafanya kazi ya kurejesha heshima yake, watu waipende tena. Mechi ya juzi Yanga inafungwa goli mashabiki wanapiga makofi, tunarudisha tunafunga la pili na la tatu na bado kuna dakika kama 900 za kucheza”
”Watu wanaleta siasa chafu na mimi nasema hizi ni takataka. Mbona kampuni kama Emirates inadhamini vilabu vingi tu vinacheza Champions League. Ina maana Arsenal wakicheza na AC Milan utasema mmoja amwachie mwenzake?”
Eng. Hersi Said Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM.