Kikosi cha Young Africans kimewasili salama Jijini Dar es salaam kikitokea Jijini Dodoma, ambako jana Jumapili (Mei 15) kilicheza dhidi ya Dodoma Jiji FC katika Uwanja wa wa Jamhuri.
Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu iliongeza alama tatu muhimu kupitia mchezo huo, kwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Dickson Ambundo na Mohamed Yusuph aliyejifunga.
Baada ya kuwasili jijini Dar es salaam, Makamu Mwenyekiti Wa Kamati Ya Usajili ya Young Africans Eng.Hersi Said alizungumza na waandishi wa Habari Uwanja wa Ndege wa Kimatafa wa Julias Nyerere.
Hersi amesema hawana budi kumshukuru M/Mungu kwa kupata ushindi dhidi ya Dodoma Jiji FC, na kwa sasa wanaendelea na mpango kujiandaa na mchezo ujao.
“Tunamshukuru M/Mungu kwa kupata ushindi dhidi ya Dodoma Jiji FC, mchezo ulikua mgumu sana na ulikua na ubora wa hali ya juu. Uwanja haukua rafiki kwetu lakini bado tulipambana na kupata alama tatu.”
“Tunawapongeza wachezaji wetu kwa kupambana, pia mashabiki wetu ambao walijitokeza kwa wingi Uwanja wa Jamhuri kuishangilia timu yao, hasa baada ya kupata matokeo ya sare katika michezo mitatu mfululizo.”
“Matokeo haya yameturudisha kwenye ramani ya kutimiza lengo letu msimu huu, kwa hiyo kila mmoja anapaswa kupongezwa na tunaamini mambo yataendelea kuwa mazuri hadi mwishoni mwa msimu huu.” amesema Eng.Hersi Said
Young Africans inaendelea kuwa kileleni kwa kufikisha alama 60, ikifuatiwa na Bingwa Mtetezi Simba SC yenye alama 49 katika msimamo wa Ligi Kuu.