Klabu za Arsenal na Chelsea zote za jijini London-England, zimefikia makubaliano ya Biashara ya usajili wa Kiungo kutoka nchini Italia Jorge Luiz Frello Filho Cavaliere ‘Jorginho’.
Klabu hizo zimefikia makubaliano hayo, ambayo yatagharimu Pauni Milioni 12 sawa na Dola za Marekani 14.8 kama ada ya uhamisho wa Kiungo huyo kutoka The Blues kwenda The Gunners.
Jorginho mwenye umri wa miaka 31, alitarajiwa kufika kwenye Uwanja wa mazoezi wa Arsenal majira ya Mchana kwa saa za England, kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kukamilisha taratibu zote za kujiunga na Miamba hiyo ya Kaskazini mwa jijini London.
Endapo mambo yatakwenda sawa, Jorginho atasaini mkataba na Klabu ya Arsenal hadi mwaka 2024, ambao utakuwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa Klabu ya Arsenal imelazimika kuhamishia nguvu za usajili kwa Kiungo huyo, baada ya Dili la kumsajili Moises Caicedo kukwekwa kapuni na Klabu ya Brighton & Hove Albion mwishoni mwa juma lililopita.
Wakati Jorginho ajipanga kuhama mitaa huko London, Klabu ya Chelsea nayo inatajwa kukimbizana na muda, ili kufanikisha usajili wa Kiungo kutoka nchini Argentina na Klabu ya Benfica ya Ureno Enzo Fernandez.
Chelsea imejipanga kukamilisha usajili wa Kiungo huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Argentina kilichotwaa Ubingwa wa Dunia nchini Qatar mwaka 2022, kabla ya kufungwa kwa Usajili wa Dirisha Dogo majira ya saa sita usiku kwa saa za England.