Mkurugenzi wa michezo wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Eric Abidal, amesema walikua na mpango wa kumsajii mshambuliaji kutoka Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, wakati wa dirisha dogo la usajili (Mwezi Januari), lakini waliamua kusitisha mpango huo.
Aubameyang amesaliwa na mkataba wa miezi 18 (sawa na mwaka mmoja na nusu) kuitumikia Arsenal ya England, ambayo ilimsajili Januari 2018 akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Abidal amesema jina la mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, lilikuwa kwenye orodha ya wachezaji waliokua wamepanga kuwasajili mwezi Januari, lakini siku chache kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili klabu ilifanya maamuzi ya kuachana na mpango huo.
Hata hivyo Abidal ameshindwa kueleza wazi kama wataendelea na mpango wa kumuwania mshambuliaji huyo wakati wa majira ya kiangazi (mwishoni mwa msimu huu), lakini akasisitiza FC Barcelona itafanya usajili kwa wakati huo.
“Ninamfahamu vizuri. Aubameyang ni mchezaji mzuri na mwenye viwango vya kucheza kwenye kikosi cha FC Barcelona. Lakini tulisitisha mpango wa kumsajili mwezi Januari.”
“Ilipangwa awe sehemu ya kikosi chetu, lakini tutaangalia mwishoni mwa msimu huu, kama tutaweza kufanikisha lengo la kukiboresha kikosi chetu ili kiwe bora zaidi ya kilivyo sasa.”
Kwa msimu huu Aubameyang anaongoza kwa upachikaji mabao kwenye kikosi cha Arsenal, baada ya kufanya hivyo mara 14, huku kwenye orodha ya wafungaji bora mpaka sasa akishika nafasi ya tatu sawa na Danny Ings wa Southampton, Marcus Rashford wa Manchester United na Mohamed Salah wa Liverpool.
Nafasi ya kwanza kwenye orodha ya kupachika mabao mpaka sasa kwenye ligi ya England inashikwa na mshambuliaji wa Leicester City Jamie Vardy kwa kupachika mabao 17, akifuatiwa na Sergio Agüero wa Manchester City mwenye mabao 16.