Msanii wa Sanaa ya uchekeshaji kutoka nchini Kenya Erick Omondi amekamatwa na jeshi la Polisi Nchini humo na kupelekwa katika kituo kikuu cha jeshi hilo mjini Nairobi kufuatia maandamano aliyoyafanya mbele ya Bunge la Kenya.
Omondi ametiwa mbaroni akiwa mita chache kutoka eneo la Bunge la nchi hiyo wakati akijaribu kuandamana kwa madai ya kupambania haki za wasanii wa muziki nchini Kenya kwa kushinikiza wasanii hao wapewe kipaumbele kuanzia kwenye upande wa matamasha mpaka kazi zao kuchezwa kwenye vituo mbali mbali vya Radio na Televisheni.
Jambo ambalo amekuwa akilizungumza mara kadhaa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, kuhusu kuzorota kwa maendeleo ya Sanaa ya Muziki na wasanii nchini humo, ukilinganisha na wasanii wa Mataifa mengine ya Afrika.
Siku ya Jana Nov 15, Omondi alikaririwa akitoa maneno ya kuhamasisha jambo hilo kabla ya kuanza maandamano hayo mapema leo Novemba 16,2021.
“Kesho tunaenda Bungeni kupigania muziki kwa sababu huko ndio kuna Spika!!!. Lakini hekima yangu itaniua siku moja, Kesho tukutane Bungeni kupigania Muziki wetu kwa sababu huko ndiko kuna Spika” alisema Omondi.
Katika Video inayosambaa mitandaoni Eric ameonekana akiandamana mita chache mbele ya Bunge la nchi hiyo, hata hivyo maandamano hayo hayakwenda mbali punde baada ya kuvamiwa na jeshi la polisi na kumkamata.
Licha ya kuandamana kwa dhamira ya kupigania haki za wasanii wa muziki wa Kenya, mpaka sasa hakuna msanii yeyote wa muziki kutoka nchini humo, aliyejitokeza kusisimama naye isipokuwa rapa KRG the Don ambaye ameapa kuwa atakwenda kumuona Eric Omondi katika kituo cha polisi.
“Eric Omondi amekamatwa mjini akipigania wanamuziki, sijaona, yaani hakuna mwanamuziki aliyesimama naye….niko njiani naelekea mjini kuhakikisha Erik Omondi anaachiliwa ndani ya Saa mbili” alisema KRG.
Ni kwa takribani wiki mbili sasa tangu mchekeshaji huyo kuanzisha kampeni maalumu yenye lengo kupambania haki za wasanii kwa kuibua mijadala kuhusu kudorora kwa tasnia ya muziki wa Kenya huku akizitupia lawama zake kwa wadau mbali mbali wa tasnia hiyo wakiwamo baadhi ya wasanii kwa kukosa kusimama thabiti na kuupambania muziki wa Kenya.