Mlinda Lango wa Geita Gold FC, Erick Johora ameitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichosafiri kwenda Tunisia kuweka kambi kwa ajili ya mechi ya kuwania kufuzu fainali za Afrika (AFCON) 2023.
Kikosi hicho, chini ya Kocha Mkuu, Adel Amrouche kitakuwa na kazi ya kutafuta alama tatu au sare ili kuhakikisha inafuzu mbele ya Algeria iliyo na tiketi mkononi.
Kikosi hicho kina maingizo mapya akiwemo Clement Mzize, Johora huku kiungo Jonas Mkude akirudishwa ilihali Feisal Salum, Mohamed Hussein na Shomari Kapombe wote wakitemwa.
Johora amesema amejisikia fahari kuitwa na kufichua huenda kucheza vyema mechi mbili za Ligi na kutoruhusu bao kimembeba mbele ya Amrouche, kitu ambacho hakijawahi kutokea alipokuwa Young Africans.
Amesema alipokuwa Young Africans hakuwahi kuitwa Taifa Stars kwa vile alikosa namba mbele ya Djigui Diarra.
“Sikupata nafasi ya kucheza Young Africans, ila sasa nimeonekana pengine kocha aliona nilichokifanya, nimefurahi kwani ilikuwa ndoto yangu kuitwa, japo hakutarajia kama ingekuwa mapema namna hii,” amesema Johora.