Imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, ameanza kukisuka kikosi anachokihitaji, baada ya kuongea na kiungo mkabaji kutoka nchini Chad, Erick Mbangossoum, ili ajiunge naye katika kipindi cha Dirisha Dogo la usajili.
Taarifa zinaeleza kuwa Benchikha alizungumza na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 na kimo cha mita 1.85, nchini Morocco wakati akiwa na kikosi cha Simba SC kilipokwenda kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo pamoja na mambo mengine alikutana naye na baada ya hapo akaongea na uongozi wake kwani moja ya mapungufu yaliyopo kwenye kikosi ni kutokuwa na kiungo mkabaji asilia.
Chanzo kinaeleza kuwa Benchikha alipata urahisi kwa kuteta na kiungo huyo kwani anacheza soka la kulipwa nchini Morocco katika Klabu ya Union Touarga Sport yenye maskani yake Rabat ikishiriki Ligi Kuu Morocco na kwa sasa ikishika nafasi ya 10 baada ya kujikusanyia pointi 14 katika michezo 10 kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
“Hana wasiwasi naye kwa sababu wanafahamiana, amemwambia aje Simba SC amfanyie kazi na tayari kocha ameshauambia uongozi na makubaliano yameshafanyika, thamani yake ni kulipa zaidi ya dola 235,000 sawa kiasi cha Sh. milioni 587 za Kitanzania hivi. Kwa sasa kuna mazungumzo tu ya kwanza yalipwe kwa awamu ngapi,” kilisema chanzo hicho kikimzungumzia kiungo huyo aliyejiunga na Union Touarga Sport tangu Juni 2020.
Taarifa zinaeleza kuwa mpango utakapokamilika kwa asilimia 100, mchezaji huyo atafanyiwa vipimo vya afya nchini Tunisia na kusaini mkataba mrefu wa miaka mitatu.
“Baada ya hapo atasafiri kuja Tanzania na sisi tunakwenda kumsubiri Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wasije kumuiba bure,” alitania mtoa taarifa hizi.
Simba SC imekubali kumchukua mchezaji huyo kwa sababu atacheza moja kwa moja Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kwani timu yake haikushiriki michuano yoyote inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani humo kwani msimu uliopita ilimaliza nafasi ya nane.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa awali Benchikha alitaka kuongeza wachezaji sita, lakini sasa ameongeza mpaka kufikia tisa wapya ambao wataongezwa kwa awamu, kipindi cha dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu ambapo wataongezwa wachezaji kadhaa na msimu ujao kutafanyika usajili mwingine wa kumalizia idadi inayotakiwa.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, alipoulizwa ili kuthibitisha mipango hiyo, amesema tayari kipindi cha usajili kinakuja hivyo tetesi hizo ni lazima zitakuwapo.
Amesema yeye anavyofahamu bado wanaendelea kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na sasa wanarejea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo mpaka sasa hajui chochote kuhusu usajili na kama chochote kitatokea basi hatosita kuwaeleza Wanachama na Mashabiki wa timu hiyo.
“Hiki ndicho kipindi chenyewe, tetesi zitakuwa nyingi sana mwisho wa siku wachezaji watakaosajiliwa watajulikana na kuonekana, sasa hivi sina chochote cha kuwaambia Wanasimba zaidi ya kukusanya nguvu zetu kwenda kuishangilia timu yetu, kwa sasa imeanza kutupa matumaini na nguvu mpya, kocha Benchikha naye ameleta mapinduzi mapya na amewaita mashabiki wajazane viwanjani, naomba turudi uwanjani kwa sababu mpira wetu ule tunaoupenda umerudi,” amesema Ahmed.
Keshokutwa ljumaa (Desemba 15) Simba SC itacheza dhidi ya Kagera Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu, kabla ya kurudiana na Wydad Casablanca, Jumanne (Desemba 19) ukiwa ni mchezo wa Mzunguuko wanne ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.