Meneja wa Kikosi cha Manchester United Erik ten Hag amemtetea Mlinda Lango David De Gea licha ya uzembe wake uliosababisha kupoteza mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya West Ham United Jumapili (Mei 07).
Mlinda Lango De Gea yuko kwenye mazungumzo kuhusu mkataba mpya pale Old Trafford, lakini aliruhusu kombora la Said Benrahma kutoka umbali wa yadi 20 liruke juu ya glovu zake na kuiwezesha West Ham kuibuka na ushindi wa 1-0.
Kwa matokeo hayo Manchester United wako mbele kwa alama moja pekee dhidi ya Liverpool inayosonga mbele kwa kasi, ingawa wana mchezo mmoja mkononi, baada ya kushindwa kwa mara ya nane wakiwa ugenini msimu huu na mara ya pili ndani ya siku nne kufuatia kupoteza katika dakika za mwisho kutoka kwa Brighton.
“Inafadhaisha? Ndio, nimeiona kwa njia ile ile. Nadhani tulianza vizuri, tulipanga mchezo, tukatengeneza nafasi, hatukuchukua na kisha tukatengeneza kosa moja,” alisema Ten Hag.
“Makosa mara mbili ya mtu binafsi na unapoteza michezo. Lakini ndivyo ilivyo. Sasa tuna wiki nzima, tunapaswa kujipanga upya na kuendelea.
“(De Gea) ndiye ambaye hajafungwa mabao zaidi kwenye Ligi Kuu, tusingekuwa katika nafasi hii bila yeye. Hakuna wasiwasi. Tunataka abaki na kuongeza mkataba wake.”
“Hakuna kilichobadilika. Tungeweza kuifanya iwe rahisi kwa ushindi. Tunahitaji ushindi kila kitu kiko mikononi mwetu.”