Gary Neville amemuonya Erik ten Hag kuwa atafutwa kazi hapo Manchester United, huku Mholanzi huyo akikabiliwa na hatima ya watangulizi wake kwa sababu ameshindwa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri.
Man United imetupwa nje ya Kombe la Carabao baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 nyumbani kutoka kwa Newcastle juzi Jumatano (Novemba Mosi) usiku ikiwa ni siku tatu baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Manchester City kwa idadi kama hiyo ya mabao.
Ten Hag sasa anashuhudia mwanzo mbaya zaidi wa msimu kwa Man United tangu msimu wa mwaka 1962-63 na klabu hiyo tayari imepoteza mechi tano kati ya 10 za nyumbani kwenye Uwanja wa Old Trafford ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1930-31.
Neville alidokeza kuwa Ten Hag atatimuliwa hapo Man United endapo timu hiyo itaendelea kufanya vibaya katika Ligi Kuu ya England pamoja na mashindano mengine.
Man United ilimaliza ya tatu katika msimu wa kwanza wa kocha Mholanzi kuifundisha timu hiyo.
Beki huyo wa zamani wa kulia wa Man United ameonya kuwa mwenendo mbaya wa kocha huyo huenda ukamsababishia kutupiwa virago.
Aidha, kocha huyo anasema kuwa pamoja na nafasi mbaya ilipo klabu hiyo, lakini yeye bado anaamini kuwa ndiye mtu sahihi zaidi wa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri.
Ushindi huo wa mabao 3-0 ni wa kwanza mkubwa kwa Newcastle United ugenini dhidi ya Manchester United kwa miaka 93.
Ukiangalia mchezo wa Jumapili (Oktoba 29) iliyopita dhidi ya majirani zao Man City, ulikuwa ni wa kwanza kwa United kupoteza nyumbani kwa mabao matatu au zaidi tangu Oktoba 1962.