Viongozi wa Ethiopia na Eritrea hatimaye wamesaini makubaliano ya kumaliza vita na uhasama kati ya nchi hizo na kuanza utekelezaji.
Mkutano kati ya Rais wa Eritrea, Isaias Afewerki na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed uliozaa matunda hayo, ulifanyika wiki hii jijini Asmara nchini Eritrea na kuweka rekodi kuwa mara ya kwanza viongozi wa ngazi za juu wa nchi hizo kukutana katika kipindi cha miaka takribani ishirini.
Makubaliano hayo yaliyoonesha matumaini ya kutekelezeka yamemaliza mgogoro wa mpaka kati ya nchi hizo na kuyafanyia kazi makubaliano ya awali ya mwaka 1998-2000 ambayo hayakuwahi kutekelezwa, hali iliyoendeleza taharuki kati ya majirani hao.
Katika makubaliano hayo, viongozi hao pia wamekubaliana kufungua mipaka na kuanza kufanya biashara ya pamoja na kujenga balozi katika nchi zao.
Familia ambazo zilitengana kutokana na mgogoro huo kwa mara ya kwanza jana zilipata nafasi ya kuanza kuwasiliana kwa njia ya simu tangu vita ilipoanza.
Mmoja kati ya waliopata nafasi ya kuwasiliana na ndugu yake ni mwandishi wa BBC, Shishay Wores ambaye ni raia wa Ethiopia akiwasiliana na kaka zake walioko Eritrea.
“Kwa muda huo [nilipompigia kaka yangu simu] moyo wangu ulisimama, sauti yangu ilitetemeka na nilihangaika kuyatafuta maneno. Ilinichukua muda kutulia na kuzungumza na kaka,” Wores alisimulia.
Tangu mwaka 2000, nchi hizo mbili zilikuwa katika hali ya kutokuwa na vita ya moja kwa moja lakini pia hakukuwa na amani kati ya nchi hizo, huku kila nchi ikiiwekea vikwazo nchi nyingine na kuituhumu kwa masuala mbalimbali ya kuihujumu.