Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland amefunguka kuwa anajiamini binafsi kuwa ana nafasi ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or mbele ya mpinzani wake na mtetezi wa tuzo hiyo, Lionel Messi.
Mshambuliaji huyo amesema hayo ikiwa ni baada ya kupita siku chache tangu alipochaguliwa kuwania tuzo hiyo akiwa sambamba na Messi, Vinicius Jr, Jude Bellingham, Karim Benzema na mastaa wengine. Mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa Oktoba 30, mwaka huu.
Haaland anapewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo baada ya kuwa na msimu mzuri akiwa na Man City msimu uliopita ambapo alibeba mataji matatu ‘Treble’ huku pia akichukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Kiume wa UEFA kwa msimu uliopita.
Akizungumzia juu ya kubeba tuzo hiyo, Haaland alisema: “Ninajiamini binafsi, ipo hivyo. Ninajua kuna vitu natakiwa kuviboresha zaidi, lakini bado ni kijana mdogo. Lakini ndiyo, nina nafasi mwaka huu.”