Mshambuliaji kutoka nchini Norway Erling Haaland amesema malengo yake makubwa ni kuelekea kuweka historia akiwa na Manchester City inayofukuzia kushinda mataji matatu msimu huu.
Mshambuliaji huyo alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Soka jijini London, juzi Alhamis (Mei 25).
Haaland amefunga mabao 52 katika mechi 51 akiwa na City kabla ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu England utakaochezwa leo dhidi ya Brentford.
City itacheza dhidi ya Inter Milan mjini Istanbul, Uturuki katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Juni 10, ikiwa ni juma moja baada ya kucheza dhidi ya Manchester United kwenye fainali ya Kombe la FA, wakiwa tayari wameshinda taji la EPL.
Wanalenga kuiga mafanikio ya wapinzani wao wa jiji moja Manchester ambao walibeba mataji matatu mwaka 1999.
Haaland amesema: “Zimesalia fainali mbili, tunapaswa kukaa macho ingawa tulishinda Ligi Kuu.
“Lazima tuwe makini ili kufikia kile tunachoweza kufikia katika fainali mbili zijazo. Nitafanya kila niwezalo kufikia mambo mazuri kwenye fainali na natumaini nitashinda zote mbili.”