Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, ameieleza mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kuwa ndoa yake na mumewe, Gustavus Babile haijavunjika na anaishi Mbweni, Jijini Dar es salaam.
Bulaya alibainisha hayo jana mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba, alipokuwa akijibu maswali aliyoulizwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Simon Wankyo.
Alidai kuwa yeye na mumewe walifunga ndoa mwaka 2003, Halima Mdee ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo ni jarani yake huko Mbweni wanakoishi sasa.
Bulaya alitoa maelezo hayo wakati akitoa utetezi wake katika kesi inayomkabili na viongozi wengine wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe.
Akihojiwa na wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi kuhusu hati yake ya kusafiria, Bulaya alibainisha kuwa katika hati hiyo hakuna mahali popote palipogongwa muhuri pakionesha alisafiri nje ya nchi kati ya Februari 16 hadi 28 mwaka 2018.
Ameieleza Mahakama kuwa, Februari 16, 2018 aliwahi kuondoka katika mkutano wa kufunga kampeni kwa kuwa Halima alikuwa anaumwa, hivyo walienda kujiandaa na safari ya kwenda kwenye matibabu nchini Afrika kusini.
Katika hatua nyingine alieleza kuwa hakuna sheria inayoruhusu chama cha siasa kuhamasisha wafuasi wake kudai haki kwa maandamano au vurugu.
Kesi hiyo iliahirishwa mpaka Januari 20 hadi 24 mwakani, ambapo shahidi wa 10 wa upande wa utetezi anatarajiwa kutoa ushahidi wake.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Naibu katibu Mkuu Zanzibar, Salumu Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Vicent Mashinji, Mbunge John Heche na Ester Matiko.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13, likiwemo la kula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko la kutawanyinka.