Aliyekuwa mbunge wa viti maalum CCM, mkoa wa Mara, Ester Bulaya ametangaza kutogombea ubunge kupitia chama hicho, hivyo nguvu zake za kuelekea bungeni atazielekeza katika chama kingine cha siasa.

Bulaya ameweka wazi uamuzi wake huo ikiwa ni siku moja baada ya zoezi la kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali kupitia CCM kuhitimishwa nchi nzima.

Hata hivyo, Bulayo hakuweka wazi chama anachotarajia kuhamia ingawa taarifa za awali zinaeleza kuwa anaweza kutimkia chama kimojawapo kati ya vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).

Mwanasiasa huyo aliyekuwa na nguvu ya ushawishi wa hoja alipokuwa bungeni, awali alieleza kuwa na mpango wa kugombea ubunge wa jimbo la Bunda kupitia chama hicho huku akitarajia kuchuana na mbunge wa jimbo hilo, Stephen Masato Wasira.

Bulaya anakuwa mbunge wa pili wa CCM kutangaza kukitosa chama hicho baada ya hatua kama hiyo kuchukuliwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.

Wakati hayo yakiendelea, hali inaendelea kuikaba koo CCM ambapo katika jimbo la Monduli lililokuwa likishikiliwa na Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Edward Sapunyo amebariki uamuzi wa madiwani 20 kuhamia Chadema kwa kile walichodai kutoridhishwa na uamuzi na chama hicho kuliondoa jina la Lowassa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais.

Mastaa Wawili Watangaza Kupata Watoto Kwenye Tuzo Za MTV/MAMA2015
‘Safari Ya Matumaini Yahamia Ukawa’