Mgombea ubunge wa jimbo la Bunda Mjini kwa tiketi ya Chadema, Esther Bulaya alikamatwa na jeshi la polisi mjini humo na kulazwa selo kwa tuhuma za kutaka kuvamia kituo cha polisi.

Bulaya alikamatwa juzi mjini Bunda na kusafirishwa hadi mjini Musoma ambapo alilazwa selo lakini jana aliachiwa kwa dhamana.

Mwanasheria wa mgombea huyo, Peter Makole alisema kuwa mteja wake anatarajiwa kufikishwa mahakamani na anakabiliwa na kesi ya kutaka kufanya jaribio la kuvamia kituo cha polisi.

Hata hivyo, Mwanasheria huyo alikanusha tuhuma hizo na kueleza kuwa ni njama zinazofanywa na wapinzani wake kwa lengo la kudhoofisha harakati zake kisiasa.

Alieleza kuwa Bi. Bulaya alifika katika kituo cha polisi Bunda Mjini, juzi majira ya saa 11 jioni kwa lengo la kutaka kumona Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Kaunya Yohana, aliyekuwa akishikiliwa kituoni hapo na alitaka kuhoji sababu za kukamatwa kwake.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya kuachiwa kwa dhamana, Bi. Bulaya aliungana na kauli za mwanasheria wake huyo na kudai kuwa tukio hilo ni sehemu ya njama za mahasimu wake wa kisiasa kutaka kumchanganya na kumdhoofisha.

 

Huyu Ndiye ‘Star’ Aliyevunja Rekodi Ya Instagram Duniani
Video: Lowassa Alivyoiteka Arusha, Habari Kamili Iko Hapa