Gwiji wa Klabu ya Arsenal ya England Lauren Etame Mayer amesema kikosi cha klabu hiyo kinapaswa kufikisha alama 10/10, endapo inataka kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kwa mara ya kwanza tangu 2004.
Mkongwe huyo anaamini Manchester City ilipunguza uwiano wa alama baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Southampton, huku Arsenal ikiambulia sare ya mabao 2-2 na Liverpool.
Lauren ambaye aliwahi kukipiga Arsenal amesisitiza matokeo mabovu kama hayo kipindi hiki yatawatibulia mipango yao wakianza dhidi ya West Ham kwenye mchezo mwingine utakayochezwa mwishoni mwa juma hili.
Akizungumza kuhusu kiwango cha Arsenal, Lauren 46, amesema: “Kwa sasa naipa Arsenal alama 9/10 kwa sababu bado presha ni kubwa, lakini kama wanataka kubeba ubingwa wanatakiwa kupata alama 10/10. Wanachotakiwa ni kushinda kila mechi. Nimesikitika kwa sababu hawakupata alama tatu Anfield.”
Licha ya Gabriel Martinelli na Gabriel Jesus kuipa Arsenal mabao mawili ya kuongoza, Mohamed Salah na na Roberto Firmino waliwatibulia na mchezo kumalizika kwa maba 2-2.