Shirikisho la soka nchini Ethiopia (EFF) limethibitisha timu ya taifa ya nchi hiyo haitoshiriki michuano ya Afrika mashariki na kati (CECAFA Senior Challenge Cup), itakayoanza mwishoni mwa juma hili nchini Uganda.
Hatua ya kutangaza kuiondoa timu kwenye michuano hiyo, inadhihirisha mchezo dhidi ya majirani zao Eritrea, hautokuwepo kwa mwaka huu, baada ya kupangwa kundi moja.
Mbali na kuthibitisha kuiondoa timu ya taifa ya wanaume kwenye michuano hiyo, pia EFF haitopeleka timu ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, ambayo ilitakiwa kushiriki michuano ya ukanda huo itakayofanyika Uganda.
Hata hivyo hadi EFF wanathibitisha kuziondoa timu zao kwenye michuano ya CECAFA, walikua hawajatoa sababu maalum za kufanya hivyo.
Chanzo cha habari hizi kimeeleza kuwa, huenda matatizo ya kifedha yakawa sababu kwa viongozi wa EFF kuridhia timu zao zisishiriki michuano ya ukanda wa Afrika mashariki na kati.
Ethiopia na Eritrea hazijawahi kukutana katika ngazi ya timu za taifa za wakubwa, tangu mataifa hayo yalipoingia katika vita vya uhasama mwaka 1998.
Mahusiano baina ya nchi hizo, yalianza kurejea katika hali ya kawaida mwaka jana, na endapo zingekutana katika mchezo wa soka kupitia michuano ya CECAFA mwaka huu ingekua mara ya kwanza, na huenda ingetumika kuhamasisha ushirikiano mwema.
Mwanzoni mwa mwaka huu Ethiopia, pia walitangaza kuiondoa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 ya CECAFA iliyofanyika nchini Eritrea.
Kujiondoa kwa Ethiopia katika michuano ya (CECAFA Senior Challenge Cup) kunadhihdirisha kundi A linasaliwa na timu tatu ambazo ni wenyeji Uganda, Burundi na Eritrea.