Bunge la Ethiopia limemchagua Sahle-Work Zewde kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo ambayo inatajwa kuwa moja ya vielelezo vya mataifa ya Afrika ambayo hayakutawaliwa rasmi na wakoloni.
Rais Sahle-Work Zewde, anatajwa kuwa mwanadiplomasia mzoefu mwenye heshima kubwa ndani ya nchi hiyo na nchi alizofanya kaz. Anaweka historia ya kuwa Rais pekee mwanamke aliyeko madarakani hivi sasa katika bara la Afrika.
Amechaguliwa na Bunge ikiwa ni wiki moja tu baada ya Waziri Mkuu, Abiy Ahmed kutangaza baraza lake la mawaziri ambalo nusu ya wajumbe wake ni wanawake.
Akizungumza jana baada ya kuapishwa, Rais Sahle-Work ameahidi kuhakikisha kuwa suala la usawa kati ya wanawake na wanaume linakuwa na uhalisia katika nchi hiyo.
Aidha, aliahidi kuhakikisha anaweka juhudi kwa nchi hiyo kuwa na amani kwani vita huleta athari kubwa huku muathirika wa kwanza akiwa mwanamke na mtoto.
“Ninawasihi kuhakikisha mnahamasisha amani yetu, kwa jina la ‘mama’ ambaye huwa wa kwanza kuathirika wakati ambapo hakuna amani.”
Uchaguzi wa Rais Sahle-Work umepokewa vizuri na Waethiopia hasa kwa kuangalia kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wengi wameutaja kuwa wa kihistoria.
Ingawa amekuwa Rais wa kwanza mwanamke katika nyakati hizi za sasa, wengi wamekumbuka pia enzi za mtawala wa kike wa taifa hilo, Zewditu aliyeitawala nchi hiyo mwanzoni mwa karne ya 20.