Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Etienne Ndayiragije amewatoa hofu mashabiki wa soka nchini, kuhusu kutokuwepo kwa beki Erasto Nyoni, ambaye hakusafiri na timu kuelekea Monastir, Tunisia kwa ajili ya mchezo wa pili wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021) dhidi ya Libya.
Nyoni alikumbwa na majeraha akiwa katika majukumu ya mchezo wa awali wa kundi J dhidi ya Equatorial Guinea siku ya Ijumaa, ambapo Taifa Stars waliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja.
Kocha Ndayiragije amesema tayari ameshajipanga kuziba pengo la beki huyo wa klabu bingwa Tanzania bara Simba SC, na anaamini hakutokua na madhara yoyote katika safu ya ulinzi ya Taifa Stars katika mchezo dhidi ya Libya, ambao utachezwa leo majira ya saa nne usiku.
Amesema amejipanga kuwatumia Kevin Yondani na Bakari Mwamnyeto kama mabeki wa kati, baada ya kuona ushirikiano wao ukileta mafanikio makubwa, kwenye mchezo wa awali wa kundi J, dhidi ya Equatorial Guinea.
“Ni kweli tunammiss Nyoni, lakini sina budi kupanga mikakati mbadala ambayo itakisaidia kikosi cha Taifa Stars kupambana dhidi ya wapinzani wetu,” amesema Ndayiragije.
“Kiujumla timu ipo vizuri na tumejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mpambano wetu wa pili wa kundi J, nina uhakika tutapambana hadi dakika ya mwisho kwa ajili ya kuendeleza harakati za ushindi.”
Taifa Stars inawania nafasi ya kufuzu kwa mara ya pili mfululizo kwenye fainali za mataifa ya Afrika, baada ya kushiriki michuano hiyo mwaka huu 2019 nchini Misri.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilishiriki fainali hizo mwaka 1980 nchini Nigeria, na ililazimika kusubiri kwa miaka 40.