Umoja wa Ulaya (EU), umesema hii leo kwamba rais Alexander Lukashenko sio kiongozi halali wa Belarus na kwamba hatua ya kuapishwa haraka Lukashenko kuingia madarakani ni kitendo kilichokwenda kinyume na matakwa ya wananchi wa Belarus.

Taarifa ya pamoja ya nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya iliyotolewa imebaini kwamba kile kilichoitwa kuapishwa madarakani, na mamlaka mpya yanayodaiwa na Lukashenko yanakosa uhalali wa kidemokrasia wa aina yoyote.

Taarifa hiyo imekwenda mbali zaidi na kueleza kwamba kuapishwa huko kwa Lukashenko kunakwenda kinyume na matakwa ya sehemu kubwa ya idadi ya watu wa Belarus kama ambavyo imejionesha kupitia maandamano makubwa ya umma nchini humo.

Agosti 9 mwaka huu, nchi hiyo ilifanya uchaguzi mkuu ambapo kwa mujibu wa matokeao rasmi Rais Lukashenko alitangazwa kuwa mshindi matokeo ambayo yalisababisha maelfu kukusanyika wakitaka Rais Lukashenko kuondoka madarakani licha ya uwepo wa Polisi katika eneo hilo.

Lukashenko amekuwa rais wa Belarus kwa miaka 26 sasa na alishinda uchaguzi wa Agosti mwaka huu kwa zaidi ya 80%, huku mgombea wa upinzani, Svetlana Tikhanovskaya alipata 10% ya kura zilizopigwa.

KMC FC kucheza na Kagera Sugar kesho Kaitaba
Kipaumbele cha wizara ya afya katika nafasi za ajira