Serikali imesema katika kipindi cha pili cha awamu ya pili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli itajikita zaidi katika kuboresha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, katika kujenga uchumi wa nchi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi, ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini,Frederic Clavier.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa baada ya kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Magufuli kujikita katika uwekezaji mkubwa wa maeneo ya miundombinu na nishati pamoja na huduma za kijamii sasa serikali inalenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi.

Balozi wa Ufaransa nchini Frederic Clavier, amemkabidhi Prof. Kabudi barua ya iliyoandikwa na  Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron  kwenda kwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli kumpongeza kwa kuiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ikiwa ni miaka mitano kabla ya muda uliopangwa.

Aidha, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Manfred Fanti, ambaye amemueleza Kabudi kuwa  pamoja na kamati ya mambo ya Nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya kujadili masuala mbalimbali yanayoihusu Tanzania, bado hakuna maazimio yeyote yaliyofikiwa kuhusu Tanzania na kwamba Umoja wa Ulaya utaendelea kuimarisha mahusiano mazuri na ya kihistoria yaliopo kati ya Tanzania na Umoja huo.

Aidha, Balozi Fanti ameihakikishia Tanzania kuwa Umoja Ulaya utatekeleza  miradi yote iliyopangwa kutekelezwa Nchini kwa ufadhili wa Umoja huo.

Katika tukio jingine, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi za Masalia ya Mauaji ya Kimbari (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT), Abubacar Tambadou.

Katika mazungumzo yao, Tambadou amemweleza Waziri Kabudi kuwa amefika kujitambulisha baada ya kupata uteuzi huo, lakini pia kuishukuru Tanzania kwa ushirikiano inaoutoa kwa Mahakama hiyo na kuomba kuendelea kutoa ushirikiano ili kuiwezesha kutimiza majukumu yake.

Rasmi Lwandamina atua Azam FC
Lule kocha mpya Mbeya City