Meneja wa klabu Tottenham Hotspur Jose Mourinho amesema ana wasiwasi na mitazamo ya baadhi ya wachezaji wake, katika kipindi hiki ambacho mapambano ya kufikia malengo yao kwa msimu huu yamepamba mto.

Mourinho alionyesha wasiwasi huo, kufautia Spurs kuambulia matokeo ya sare ya mabao matatu kwa matatu katika mchezo wa mzunguuko wa tano wa Europa League uliochezwa usiku wa kuamkia leo dhidi ya LASK.

Katika mchezo huo Mourinho aliwatumia baadhi ya wachezaji ambao hawapati nafasi ya mara kwa mara kwenye kikosi chake cha kwanza, na mwishowe walishindwa kutimiza jukumu la kupata matokeo mazuri.

Meneja huyo kutoka nchini Ureno alizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mtanange huo na kusema kuwa: “Nadhani ni suala la mtazamo, nimewahi kupitia hilo hata wakati nilipokuwa Manchester United.”

“Nilikuwa na hali kama hii tulifungwa michezo miwili ya ugenini katika hatua ya makundi. Tunapoingia hatua ya mtoano, tunakutana na wapinzani bora zaidi, michezo inakuwa ni migumu na michezo inakuwa tofauti.”

Baada ya kuulizwa kama amejifunza kitu chochote, Mourinho alisema “Hakuna jipya, uhalisia ni kwamba wachezaji wengi hawashawishiki na hatua ya makundi kwenye Ligi ya Europa. Ninalijua hilo.”

Kwa matokeo ya sare ya mabao matatu kwa matatu, Spurs inashika nafasi ya pili kwenye kundi J, kwa kufikisha alama 10, wakitanguliwa na Royal Antwerp wenye alama 12, LASK wanashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 7 na Ludogorets Razgrad wanaburuza mkia kwa kuwa na alama 0.

Mchezo unaofuata kwa Spurs kwenye michuano ya Europa League watakua nyumbani jijini London wakicheza dhidi ya Royal Antwerp, huku Ludogorets Razgrad wakiikaribisha LASK, Desemba 10.

Njaa yapelekea raia kula mchanga- Madagascar
TANAPA washindi tuzo ya dhahabu