Timu ya Soka ya Uingereza, Everton imewafunga mabingwa wa kombe la SportPesa 2017, Gor Mahia ya Kenya 2-1 katika mchezo ulioshuhudiwa na maelfu katika uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
Everton walikuwa wa kwanza kushindilia goli la kwanza nyavuni kupitia mchezaji wake mpya Wayne Rooney katika dakika ya 34 akipiga shuti kali umbali wa takribani hatua 30.
Hata hivyo, Gor Mahia walifanya purukushani zenye mahesabu mazuri na kurudisha kipigo hicho ndani ya dakika nne, hali iliyowaweka Everton mguu sawa. Magoli hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko huku timu hiyo ya Uingereza ikionekana kumiliki zaidi mpira.
Piga ni kupige iliyoambatana na makosa ya hapa na pale yaliyokuwa yanafanywa na Gor Mahia ilipelekea Everton kupata goli la pili lililowekwa nyavuni na Kieran Dowell aliyewatoka walinzi na kupiga shuti kali, hivyo kufanya matokeo kuwa 2-1 yakidumu hadi kiliposikika kipyenga cha mwisho.
Tofauti na wengi walivyotegemea, Gor Mahia walijitahidi kuwapa wakati mgumu Everton hali iliyosababisha kocha Dylan Kerr kutoa maelekezo ya mara kwa mara kwa wachezaji wake.
Rooney pia alikutana na kisiki cha kukamiwa na wachezaji wa Gor Mahia wakitimiza ahadi yao ya kumdhibiti ingawa nahodha huyo wa zamani wa Manchester Utd hadhibitiki kirahisi, hali iliyopelekea kuwapa madhara ya goli moja.