Mfuko wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Elimu haiwezi kusubirti, Education Cannot Wait (ECW), katika maeneo yenye dharura na migogoro ya muda mrefu, umetoa ombi kwa viongozi wa dunia kutoa dola bilioni 1.5 za ufadhili wa dharura, kusaidia elimu kwa watoto na wadau wake.
ECW imetoa ombi hilo katika mkutano wake wa kawaida na kusema nia ya ombi hilo ni kuweza kuwafikia watoto na barubaru milioni 20 watakaoathirika na migogoro ya aina tofauti katika kipindi cha miaka minne ijayo, sehemu mbalimbali Duniani.
Mpango huo unaotarajia kuanza mwaka 2023-2026, umeweka dhamira mpya, yenye nguvu na imara kwa mfuko huo wa ufadhili wa Umoja wa Mataifa, ambao tayari umekusanya zaidi ya dola bilioni moja na utakaosaidia moja kwa moja takriban watoto na vijana milioni 7 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016.
Hata hivyo, fedha hizo pia zinatarajia kusaidia watoto na vijana wengine wapatao milioni 31.2 katika hatua zake za vita dhidi ya janga la Uviko-19, huku tathimini ya hivi karibuni ya mfuko huo wa elimu ukisema hauwezi kusubiri kwani wasichana na wavulana milioni 222 walioathiriwa na migogoro wanahitaji msaada wa haraka wa elimu.
Zaidi ya watoto na vijana milioni 78 kati yao hawaendi shuleni, huku wengine takriban milioni 120 hawajafikia ujuzi wa chini wa kusoma au kuhesabu na kuufanya mfuko wa ECW kusema fedha za ombi hilo zitasaidia juhudi zake za kuhakikisha watoto na vijana walio katika mazingira magumu kupata elimu sawa na wengine.