Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) imejipanga kuja na mfumo wa vituo vya mafuta vinavyotembea kwa lengo la kukabiliana na ukosefu wa vituo vya kutolea huduma za mafuta maeneo ya vijijini .
Hayo yamebainishwa Novemba mosi 2019 Jijini Dodoma na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano cha mamlaka ya udhibiti wa huduma ya nishati na maji (EWURA), Titus Kaguo katika semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na mamlaka hiyo.
Amesema kuna baadhi ya maeneo hasa ya vijijini yamekuwa yana upungufu ama ukosefu wa vituo vya mafuta hivyo kusababaisha adha kwa watumiaji wa vyombo vya moto na katika kutatua changamoto hiyo EWURA imeamua kuja na mfumo mbadala.
“Kutokana na hali hiyo mamlaka inakuja na mfumo mpya wa vituo vya mafuta vinavyotembea na hii ni kutokana na uhaba wa mafuta kwa maeneo yasiyo na vituo hivyo hasa ya vijijini na hili litasaidia kama si kuondosha basi kupunguza tatizo,” amebainisha Kaguo.
Hata hivyo amesema wakati mamlaka ikiwa katika harakati za kutatua changamoto hiyo wananchi wanapaswa kuachana na tabia ya kuhifadhi mafuta kwenye makopo ya maji ama madumu huku watumiaji wa mafuta wakitakiwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa ili kujiepusha na athari zinazoweza kujitokeza.
“Kuna watu wana tabia ya kuhifadhi mafuta kwenye madumu ya maji ama chupa za plastiki ubebaji au utunzaji wa mafuta kwa mtindo huo si salama kwani ni hatari waache na badala yake wazingatie taratibu na sheria zilizowekwa ili kuepuka athari mbalimbali,” amefafanua Kaguo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) imekuwa na utaratibu wa utoaji wa elimu na semina kwa waandishi wa habari juu ya mambo mbalimbali ambapo pia imekuwa ikitahadharisha uuzaji na usafirishaji wa mafuta ya vyombo vya moto usio rasmi.