Bei za rejareja za mafuta, zilizoanza kutumika hii leo Desemba 6, 2023 zimepungua Nchini ambapo katika Mkoa wa Dar es Salaam Petrol inauzwa shilingi 3,158 kwa lita, Dizeli shilingi 3,226 na mafuta ya taa 3,423.
Tangazo hilo, limetolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA ambayo imeeleza kuwa mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Desemba yanatokana na bei za mafuta (FOB), kwenye soko la Dunia kupungua kwa wastani wa asilimia 0.86 kwa mafuta ya Petroli na asilimia 9.11 kwa mafuta ya Dizeli.
Aidha, EWURA pia imesema gharama za kuagiza mafuta kwa Bandari ya Dar es Salaam, zimepungua kwa wastani wa asilimia 24 kwa mafuta ya petroli na asilimia 30 kwa mafuta ya Dizeli huku Bandari ya Tanga gharama za kuagiza mafuta zikipungua kwa asilimia 30 kwa mafuta ya Petroli na asilimia 17 kwa mafuta ya Dizeli.
Hata hivyo, mabadiliko hayo, yanatokana na kupungua kwa bei za mafuta ghafi katika soko la Dunia kwa wastani wa asilimia 8.72 na gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 27 kwa Petroli na asilimia 23 kwa Dizeli.