Baada ya kimya cha muda mrefu kilichoambatana na tuhuma nyingi dhidi yake, 20 Percent aliyewahi kushinda tuzo 5 za Kilimanjaro kwa mkupuo, amefafanua tetesi zinazosambaa kuwa anatumia dawa za kulevya.

Akizungumzia na Dar24 Media kwenye mahojiano maalum kupitia kipindi cha Exclusive, 20 Percent amekiri kuwa amekuwa akitumia bangi lakini anaendelea kujitahidi kuachana nazo kwakuwa hazijamfanya kuwa mlevi.

“Sikufichi mimi navuta bangi, lakini mimi sio mlevi wa bangi na wala siwezi kukaa mbele za watu nikasema bangi iliruhusiwe Tanzania,” 20 percent ameiambia Dar24 Media.

“Mimi ni binadamu. Ninaposema mimi ni binadamu nina maana nina hisia zote za kibinadamu, ninasikia joto, nasikia baridi, naweza kulia naweza kucheka. Sio tu kwa sababu ni mwanamuziki ndio nicheke sehemu ya kulia au nilie sehemu ya kucheka, hapana. Kama nitakuwa na tabia hizo ni za kwangu, lakini sijawahi kuwa na tabia mbaya hata moja,” ameongeza.

Amesisitiza kuwa hajawahi kuvuta unga (cocaine/Heroine), na kwamba hata akinywa mvinyo hajawahi kulewa.

“Kwahiyo, hata kama nikinywa bia zangu mbili, unawezaje kuyumba ukinywa bia mbili… halafu bia zangu mimi sinywei baa,” amesema.

Mkali huyo wa Money Money alikuwa miongoni mwa wasanii waliotumbuiza kwenye tamasha la ‘Uhuru kuna Jambo’, lililoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi wikendi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Madawa ya kulevya ni sehemu ya tatizo linaloangamiza vipaji vya wasanii wengi nchini. Hivi karibuni baadhi ya wasanii wamejitokeza na kuwa chini ya uangalizi maalum wa matibabu. Wasanii hao ni pamoja na Ray C, Cheed Benz, Fanani wa HBC, Hawa na wengine.

Dar24 inafanya kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya. Kampeni hiyo imepewa jina la ‘Shtuka’.

Mwakyembe: Morrison ametupotezea muda
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 19, 2020