Kiungo wa klabu ya Everton Fabian Delph ameondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England, kilichoanza maandalizi ya kujiwinda na michezo ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Ulaya (Euro 2020) dhidi ya Jamuhuri ya Czech na Bulgaria.

Delph mwenye umri wa miaka 29, alipatwa na majeraha ya nyama za paja akiwa katika mchezo wa ligi kuu ya England dhidi ya Burnley, ambao walikubali kufungwa bao moja kwa sifuri, siku ya jumamosi.

Taarifa iliyotolewa na chama cha soka nchini England (FA) imeeleza kuwa: “Hakuna nafasi ya mchezaji atakaeongezwa kuchukua nafasi ya Delph katika kipindi hiki”.

Kocha mkuu wa England Gareth Southgate ataendelea kukiandaa kikosi chake, ambacho kimesaliwa na wachezaji 24.

Viungo Dele Alli wa Tottenham na Jesse Lingard wa Manchester United ni sehemu ya wachezaji walioachwa wakati kocha huyo akitangaza kikosi juma lililopita.

England inayoongoza msimamo wa kundi A, baada ya kupata ushindi mara nne, itacheza dhidi ya Jamuhuri ya Czech siku ya ijumaa (Oktoba 11), kabla ya kupambana na Bulgaria siku tatu baadae.

Uandikishaji Uchaguzi Mitaa kuanza Leo
Mwinyi Zahera: Nipo tayari kwa lolote Yanga