Aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza, Fabio Capello ameachana na shirikisho la soka nchini Urusi baada ya kukubali kuvunjwa kwa mkataba wake wa miaka mine wa kukinoa kikosi cha nchi hiyo.
Capello, mwenye umri wa miaka 69, amekubali kuondoka nchini Urusi baada ya kuafikiana na viongozi wa shirikisho la soka nchini humo suala la kusitishiwa mkataba wake kwa maslahi ya kikosi cha Urusi.

Kwa siku kadhaa viongozi wa shirikisho la soka nchini Urusi, walikuwa na vikao vya kumjadili kocha huyo kutoka nchini Italia, na maafikiano yaliyopatikana ni kuachana nae ili kumsaka kocha mpya ambaye ataweza kuivusha timu ya taifa ya nchi hiyo, na kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya za mwaka 2016.

Capello, amekuwa na matokeo mabaya katika mchakato wa kusaka nafasi ya kuelekea Ufaransa kushiriki fainali za Ulaya za mwaka 2016. Katika mchezo wa mwisho aliochezwa mwezi uliopita, Urusi walikubali kufungwa 3-0 dhidi ya Austria.

Hata hivyo, msukumo wa kuondoka kwa kocha huyo, unadaiwa kutolewa na umoja wa mashabiki wa soka nchini Urusi, ambao walionyesha kuchoshwa na matokeo mabovu, na kuutaka uongozi kumuwajibisha.

Katika harakati za kusaka nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya barani Ulaya za mwaka 2016, Urusi imepangwa kwenye kundi la saba sambamba na Sweden, Austria, Montenegro, Liechtenstein pamoja na Moldova.

Tayari Urusi imeshacheza michezo sita na kupata ushindi katika michezo miwiwli, kufungwa mara mbili na kutoka sare mara mbili hatua ambayo inaifanya nchi hiyo kufikisha point nane.

Kwa sasa Urusi inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi la saba, ikitanguliwa na nchi za Austria na Sweden na kama itashindwa kupata ushindi katika michezo minne iliyosalia na kuzipiku timu hizo mbili, mipango ya kufuzu kucheza fainali za Ulaya za mwaka ujao itakua imeshindikana.

Wingu Zito Latanda Kwa Eden Dzeko
Young Killer Kuziweka Ngoma 14 Kwenye Mixtape Mpya