Aliyewahi kuwa kocha wa klabu za Juventus, Real Madrid na timu ya taifa ya England Fabio Capello, ametangaza kustaafu shughuli za ukufunzi, akiwa na klabu ya Jiangsu Suning inayoshiriki ligi kuu ya China.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 71 ambaye waliwahi kutwaa ubingwa wa ligi ya nchini Italia mara tatu, ubingwa wa Hispania mara mbili sambamba na kuiongoza timu ya taifa ya England kwenye fainali za kombe la dunia za mwaka 2010, amesema anaamini muda wa kukaa pembeni umefika bada ya kujipima na kuona hana nafasi ya kuendelea kufundisha soka.
Capello ambaye anaendelea kukukmbukwa kwa maamuzi yake ya kujiuzulu kama kocha mkuu wa kikosi cha England miezi kadhaa kabla ya fainali za mataifa ya Ulaya mwaka 2012, pia alikifundisha kikosi cha Urusi kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.
Akizungumza katika kituo cha Radio cha Anch’io Lo Sport, kocha huyo kutoka nchini Italia ametoa shukurani kwa kila mmoja aliefanya nae kazi, sambmaba na kwa mashabiki wote wa soka waliokua wanapendezwa na utendaji wake wa kazi.
Pia amezungumzia soka la China kwa kusema lina mazingira magumu kutokana na lugha ya kichina ambayo wachezaji wengi ndio wameizoea, lakini alijitahidi kadri alivyoweza na kufanikiwa kufikia malengo ya ukufunzi wake.
“Nimejifunza mengi nikiwa hapa China, jambo kubwa lililonipa wakati mgumu nikiwa kazini ni mawasilino, ilikua vigumu kuelewana na baadhi ya wachezaji lakini ilifikia wakati tulielewana na tukafanya kazi kwa pamoja.” Amesema Capello
Kwa upande mwingine Capello ataendelea kukumbukwa kwa mazuri aliyoyafanya akiwa mchezaji wa nafasi ya kiungo katika klabu za Juventus na AC Milan kati ya mwaka 1970 na 1980s, kabla ya kuanza shughuli za ukufunzi.
Kwa matra ya kwanza gwiji huyo alianza kukinoa kikosi cha vijana cha AC Milan na baadae kupandishwa hadi katika kikosi cha wakubwa akichukua nafasi ya Arrigo Sacchi mwaka 1991.
Aliondoka Italia mwaka 1996 na kuelekea Hispania kukinoa kikosi cha Real Madrid, na baadae alirejea nchini humo bada ya kuajiriwa tena kwenye klabu ya AC Milan mwaka 1997.
Mwaka 1999 hadi 2004 alitimkia AS Roma, 2004 hadi 2006 akawa mkuu wa benchi la ufundi la Juventus, 2006 hadi 2007 alirejea Real Madrid kabla ya kuajiriwa na chama cha soka nchini England kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo mwaka 2008.
Capello alitangaza kujiuzulu kukifundisha kikosi cha England baada ya kukasirishwa na maamuzi ya kamati ya nidhamu ya chama cha soka nchini humo (FA) ya kumfungia beki na nahodha kwa wakati huo John Terry, baada ya kubainika alitoa maneno ya kibaguzi dhidi ya beki wa QPR Anton Ferdnand.