Kiungo wa AS Monaco ya Ufaransa Francesc “Cesc” Fàbregas Soler amewataja Jose Mourinho na Arsene Wenger kuwa makocha bora aliowahi kufanya nao kazi tangu alipoanza kupambana katika soka la ushindani.
Fabregas alisajiliwa na Arsenal na kutua England kwa mara ya kwanza mwaka 2003, akitokea kwenye kituo cha kulea na kukuzia vijana kinachomilikiwa na FC Barcelona La Masia.
Akiwa jijini London yalipo makao makuu ya klabu ya Arsenal, alinolewa na meneja Arsene Wenge, na aliminiwa kwa kiasi kikubwa hadi kufikia hatua ya kupewa unahodha, baada ya kuondoka kwa beki kutoka nchini Ufaransa William Gallas mwaka 2008.
Fabregas aliwataja wawili hao kama makocha bora kwake alipohojiwa na moja ya chombo cha habari nchini Hispania, ambapo alisema: “Kupata mafanikio kwenye mchezo wa soka unahitaji mapambano na kufundishwa mpira na makocha bora duniani, na ndio maana nimeanza kumtaja Arsene Wenger na Jose Mourinho.
“Najua wengi watashangaa kwa nini sijamtaja kocha wa zamani wa klabu ya Barcelona Pep Guardiola na kocha wa Timu ya taifa ya Hispania Vicent Del Bosque.
“Nikiwa Timu ya taifa ya Hispania, nimetwaa kombe la dunia mwaka 2010 Michuano ya Euro mwaka 2008 na 2012 na wakati nikiwa Barcelona nilifanikiwa kutwaa mataji sita nikiwa na Pep Guardiola, lakini bado naendelea kusisitiza Arsene Wenger na Jose Mourinho ndo Makocha wangu bora.
“Jose Mourinho na Arsene Wenger, walinilea kama mtoto wao walinifundisha mambo mengi ndani ya uwanja hadi nje ya uwanja napenda kuwashukuru sana katika karnia yangu.
“Wakati nikiwa Barcelona, Jose Mourinho alikuwa kocha Mkuu wa Real Madrid, baada ya mechi na kabla ya mechi tulikuwa tunazungumza nilivokuwa Arsenal, Jose Mourinho, alikuwa kocha Mkuu wa Chelsea na tulikuwa na mahusiano mazuri, “Alisema Fabregas.
Akiwa Arsenal kuanzia mwaka 2003 hadi 2011, Fabregas alicheza michezo 212na kufungwa mabao 35, kisha akarejea FC Barcelona kuanzia mwaka 2011hadi 2014 ambapo alifunga mabao 28 katika michezo 96 aliyocheza.
Mwaka 2014 alirejea jijini London akisajiliwa na Chelsea ambapo alicheza hadi mwaka 2019, akifunga mabao 15 katika michezo 138 na sasa yupo AS Monaco na tayari ameshacheza michezo 31 na amefunga bao moja.