Mtandao wa Facebook umefunga akaunti ya mwana harakati wa nchini Ethiopia, Jawar Mohammed.
Mwana harakati huyo ambaye akaunti zake zilikuwa zimethibitishwa (verified), amesema kuwa akaunti yake ya Facebook imefungiwa katika kipindi ambacho anaendesha harakati za kushinikiza Serikali kuwaachia huru wanasiasa inaowashikilia.
Facebook wametoa sababu kwenye akaunti yake kuwa “inaonekana kama ulikuwa unatumia vibaya akaunti yako kwa kwenda kasi kupitiliza.”
Amesema kuwa amewasiliana na kampuni hiyo tangu ilipomfungia akaunti hiyo Februari 13 mwaka huu, lakini hajapata majibu.
“Nimetumia njia zote zinazowezekana kuwasiliana nao lakini hadi sasa sijapata majibu kutoka kwao,” Jawar alisema.
Aliongeza kuwa yeye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza nchini humo kujiunga na Facebook mwaka 2005, wakati huo wanafunzi wa chuo walikuwa hawaruhusiwi kujiunga na mtandao huo wa kijamii. Hivyo, anashangazwa na uamuzi huo kwani amekuwa mtumiaji mwaminifu kwa kipindi chote akiendesha harakati za kijamii na siasa.