Mtandao wa Facebook umemfungia akaunti mwanamke mmoja anayeitwa Isis kutokana na jina lake kufanana na ufupisho maarufu wa jina la kundi la kigaidi linalojiita Islamic State of Iraq and Syria (ISIS).

Mwanamke huyo ambaye ni mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Bristol nchini Uingereza ambaye jina lake halisi ni Isis Thomas, amesimulia mkasa uliomkuta ikiwa ni wakati ambao wamiliki wa mtandao wa Facebook wamejikita katika kuhakikisha wanatokomeza mtandao wote wa kundi la ISIS na wanaowaunga mkono kupitia mtandao huo.

Alisema kuwa alikuwa akijaribu kuingiza jina lake ili aingie kwenye akaunti yake ya Facebook, ndipo alikutana na maswali ambayo hakuyategemea akitakiwa kutuma utambulisho wake halisi kwanza kabla ya kuingia.

“Walinitumia ujumbe wakasema Isis haliruhusiwi, halikidhi vigezo vya sera yao. Walinitaka kutuma utambulisho kujihakiki na nilifanya hivyo. Hiyo ilikuwa Jumatatu na sijawahi kuruhusiwa kuingia kwenye akaunti yangu tangu wakati huo,” Isis Thomas anakaririwa na gazeti la The Sun.

Katika hatua nyingine, Isis alisema kuwa huwa anajisikia vibaya kuona jina la kundi la kigaidi linalojiita Islamic States of Iraq and Syria (ISIS) linaandikwa kwenye magazeti kwa herufi ndogo hivyo kufanana na jina lake wakati walipaswa kuandika kwa herufi kubwa kwakuwa ni ufupisho wa majina.

Pamoja na misukosuko hiyo, Isis Thomas alisema kuwa hana mpango wa kubadili jina hilo alilopewa na wazazi wake ikiwa ni kumbukumbu ya kidini ya imani inayopatikana nchini Misri.

Video: Thurman Vs Porter lavunja rekodi ya ndondi, wamfuata Muhammad Ali
Maelfu waandamana London kupinga matokeo ya kura ya kujitoa EU