Wachezaji wa Simba, wamesema watakwenda kupigana kufa kupona ili kupata ushindi au hata sare kwenye mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho, hatua ya makundi dhidi ya CS Constantine ya Algeria, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids akisisitiza ni ushindi tu.
Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka keshokutwa, Jumatano kwenda kwenye mji wa Constantine kucheza mechi hiyo ya Kundi A, dhidi ya timu hiyo utakaopigwa, Jumapili saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Mohamed Hamlaoui.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mchezaji mkongwe wa timu hiyo, Mzamiru Yassin, alisema wao kama wachezaji wako kwenye mazoezi makali kwa ajili ya maandalizi kwani wanatambua hautakuwa mchezo rahisi kama wengi wanavyodhani, lakini dhamira yao ni kwenda kusaka pointi katika mchezo huo.
“Mechi ni ngumu, si nyepesi kama watu wanavyofikiria, sisi wengine ni wazoefu kwenye michuano hii, tunajua hilo, kinachotuaminisha hivyo ni kwamba mpinzani wetu tunaekwenda kucheza naye ametoka kushinda ugenini, akiifunga timu kubwa kama CS Sfaxien ya Tunisia ambayo kwenye kundi letu ndiyo ina historia nzuri ya michuano hii kuliko timu yoyote.
“Kama hao jamaa Watunisia wamefungwa kwao, ina maana si timu ya kubeza, ndiyo maana tumekomaa kwenye mazoezi,” alisema mchezaji huyo aliyejiunga na timu hiyo mwaka 2016, akitokea Mtibwa Sugar.
CS Sfaxien, imetwaa Kombe la Shirikisho Afrika mara tatu, mwaka 2007, 2008 na 2013.
Alisema wachezaji wa Simba wanatambua kuwa wapinzani wao watataka kushinda mchezo huo ili waongeze matumaini ya kusonga mbele baada ya kushinda ugenini, hivyo hawatokubali kuona hilo likitokea.
“Ni mechi ambayo wapinzani wetu wataichukulia umuhimu sana kwani wameshashinda ugenini, watataka kushinda kwao ili wawe kwenye nafasi nzuri ya kufuzu makundi, wachezaji tunajua hilo, ndiyo maana tumejiandaa kwenda kuchukua pointi tatu, ikishindikana moja kwani tayari tumeshachukua tatu nyumbani dhidi ya Bravo do Maquis, nao pia watakuja nyumbani,”, alisema mchezaji huyo anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji.
Alilisifia benchi la ufundi la timu hiyo, likiongozwa na Fadlu Davids kuwa linafanya kazi kubwa na akikiri kwa miaka ya karibuni hajaona benchi bora kama hilo.
“Nafasi ya kusonga mbele hatua ya robo fainali tunayo, ila haitoki mdomoni, bali kwa jitihada, lakini naamini tutapita kwani safari hii tuna benchi la ufundi zuri sana,” alisema.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu, amesema ushindi siku zote si zawadi bali ni kushindana, akisema huwezi kwenda uwanjani ukatarajia kushinda kama hujaandaa vizuri kikosi kwenye uwanja wa mazoezi.