Siku ya Wanawake duniani ilianza kutokana na jitihada za wanawake 15,000 mwaka 1908 walipoandamana mjini New York Marekani wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura.Kilikuwa chama cha kisoshalisti cha Amerika kilichotangaza kuwa ni siku ya kwanza ya kitaifa ya wanawake, mwaka mmoja baadae.
Wazo la kuwa siku ya kimataifa lilianzishwa na mwanamke kwa jina Clara Zetkin. Alipendekeza wazo hilo mwaka 1910 katika mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi wanawake huko Copenhagen, Denmark.
Kulikuwa na wanawake 100 hapo kutoka nchi 17 na wakakubaliana kwa pamoja. Kwa mara ya kwanza siku hii ilisheherekewa mwaka 1911, Austria, Denmark,Ujerumani na Switzerland.
Sherehe ya 100 ilifanyika mwaka 2011, hivyo mwaka huu ni sherehe ya 110 ya wanawake duniani.
Suala hilo likawa rasmi mwaka 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuanza kusherehekea siku hiyo na baadae kubuni kauli mbiu.ya kwanza mwaka 1996 ambayo ilikuwa inasema ”furahia yaliyopita, panga kwa ajili ya baadae”.
Kwanini tarehe 8 mwezi Machi. Wazo la Clara Zetkin la Siku ya kimataifa ya wanawake duniani halikuwa na tarehe maalum na haikuwa rasmi mpaka kipindi cha vita ya mwaka 1917 wakati wanawake wa kirusi walipodai Amani na kufanyia kazi tatizo la upungufu wa chakula (Waliimba Amani na Mkate).
Siku nne za mgomo, zilifanya watawala wa Urusi kuwapa wanawake haki ya kupiga kura.Tarehe ambayo mgomo ulianza ulikuwa kwenye kalenda ya Julian, ambayo ilikuwa ikitumika Urusi wakati huo, ilikuwa siku ya Jumapili tarehe 23 Mwezi Februari.
Siku hii katika kalenda ya Gregoria ilikuwa tarehe 8 mwezi Machi, na ndio hii inayosherehekewa leo.