Kisukari jina la kitaalamu hujulikana kama diabetes mellitus ni ugonjwa unaoonyesha viwango vikubwa vya sukari katika damu.

Ugonjwa wa kisukari ni mlolongo wa matatizo mwilini ya mda mrefu na mfupi kutokana na upungufu au kutoweza kutumika vizuri kwa kichocheo kinachoitwa insulin.

Insulin hutengenezwa na chembechembe zilizopo ndani ya kiungo cha kongosho. Miili yetu inahitaji insulin ili kuweza kutumia sukari tuliyonayo mwilini.

Sukari inatokana na chakula tunachokula kila siku na hutumika kwa kuupa nguvu mwilini.

Kwa kawaida sukari ikizidi, ile ziada inahifadhiwa katika ini kama mafuta. Mafuta hayo hubadilishwa kuwa sukari na kutumika wakati tukiwa na njaa kwa mda mrefu. Endapo kuna matatizo ya kutengeneza au kutumika kwa insulin, sukari mwilini huongezeka haraka na inamaanisha ugonjwa wa kisukari upo na dalili kuanza kuonekana kama zifuatazo.

  1. Kunywa maji mengi kuliko kawaida na kusikia kiu kila wakati.
  2.  Kwenda haja ndogo mara kwa mara. Watoto kukojoa kitandani.
  3. Kuwa dhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati.
  4.  Kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri.
  5.  Kusikia njaa kila wakati na kula sana.
  6.  Wanawake kuwashwa ukeni.
  7.  Kutoona vizuri.
  8.  Kupungua nguvu za kiume au hamu ya kujamiiana kwa wanawake.
  9. Ganzi, kuchomwachomwa au kutohisi unapoguswa sehemu za miguu, viganja na vidole
  10. Miguu kuoza na hata kupata gangrini.
  11.  Kukaukwa na ngozi na pia kupata aina ya ngazi katika miguu.
  12.  Vidonda au majeraha sehemu yoyote ya mwili kutopona haraka.
  13.  Majipu mwilini.
  14. Kukojoa mkojo ambao mara baada ya dakika chache hujaliwa na sisimizi.

Mara uonapo dalili hizi wahi mapema hospitali kupima ugonjwa wa Kisukari kwa ni miongoni mwa magonjwa yanayochukua muda mrefu kutibika endapo mgonjwa atachelewa kupata matibabu, pia ni miongoni mwa magonjwa ambayo huua kwa kasi zaidi nchini.

Kuna nmana tofauti ya kujizuia kupata ugonjwa wa kisukari, ikiwemo kufanya mazoezi, kula vyakula vyenye afya kama matunda, mboga za majani na kula vyakula vyenye virutubisho vyote, na mwisho kujitahidi kupima kiwango chako cha sukari mwilini ili kujua kama kuna uwezekano wa kupata ugonjwa huo ili hatua zaidi zichukuliwe.

 

Neymar: Sijawa 'fiti' kwa asilimia 100
Kauli tata za Cristiano Ronaldo zawaweka njia panda mashabiki