Hedhi ni kipindi maalumu katika mzunguko wa mwanamke mwenye umri wa kuzaa ambapo mayai yake hupevuka na huvunjika yakikosa kurutubishwa na mwanamke hutokwa na damu ukeni kwa kawaida unarudi kila baada ya mwezi mmoja.
Inakadiriwa kuwa, mwanamke hupata hedhi wastani wa mara 400 katika maisha yake na neno linalotumika sana kuwakilisha hedhi ni ‘period’, lilianza kutumika kwa mara ya kwanza kwenye miaka ya 1822 likimaanisha tukio linalotokea ndani ya muda fulani au linalojirudia baada ya muda fulani.
Mwanamke anapozaliwa huzaliwa akiwa na mayai milioni moja hadi milioni mbili. Mayai haya, mengi hufa jinsi mwanamke anavyoendelea kuishi na ni mayai 400 tu ndiyo hukadiriwa kufika hatua ya ukomavu tayari kwa uchavushwaji.
Kwa wastani, msichana huanza kupata hedhi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 12 japokuwa kuna wengine ambao huanza kupata hedhi mapema zaidi na wengine ambao huchelewa kupata hedhi yao.
Na mzunguko wa siku za hedhi huwa kati ya siku 21 hadi 35. Ingawa wengi huwa na mzunguko wa siku 28, lakini kuzidi wiki moja au kuwahi kwa wiki moja ni kitu cha kawaida.
Ifahamike kuwa msichana anaweza kupata ujauzito kabla ya kuanza hedhi yake ya kwanza. Hii ni kwa sababu, yai huanza kukomaa kabla ya kuona hedhi yake ya kwanza, hivyo kama atashiriki tendo la kujamiiana bila kinga, kuna uwezekano wa kupata ujauzito hata kabla ya hedhi kutokea.
Wanawake wengi hufikia ukomo wa kupata hedhi, kitaalamu huitwa menopause anapofikisha umri wa kuanzia miaka 48 hadi 55. Baada ya miaka huyo hatapata tena hedhi mpaka anafariki dunia japokuwa tendo la kujamiiana anaweza kulifanya, hivyo mimba haiwezi kuipata tena.
Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Afya la Epidemiology & Community Health la Uingereza lilisema kuna vyakula vinasababisha mwanamke kukoma hedhi mapema na watafiti waliwauliza wanawake mlo wao huwa una vyakula gani. Mlo wenye mboga za jamii ya kunde kwa wingi, kama vile njegere, maharage, maharage membamba na dengu kwa wastani huchelewesha ukomo wa hedhi.
Vyakula vya wanga, hasa wali na tambi, vimeelezwa kusababisha ukomo wa hedhi mapema zaidi. Wanawake ambao hedhi zao hukoma mapema wako kwenye hatari ya kupata maradhi ya moyo na maradhi ya mifupa, na wanaochelewa wanaweza kupata maradhi ya saratani ya matiti, tumbo na Ovari.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Leeds kwa wanawake 914 nchini Uingereza , pia umebaini kuwa mlo ulio na mafuta ya samaki kwa wingi na njegere na maharage unaweza kuchelewesha ukomo wa hedhi kwa wanawake.